Waumini wa Kanisa Katoliki katika ukanda wa Pwani walijumuika na wenzao ulimwenguni kuadhimisha siku ya Alhamis Kuu, inayoashiria ile karamu ya mwisho ya Yesu na mitume wake kabla hajakamatwa nakuhani mkuu wa Israeli, Yosefu Kayafa.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akizungumza na wanahabari mjini Mombasa siku ya Alhamisi baada ya ibada maalum ya Alhamis Kuu Naibu, Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo kuu la Mombasa Padri Wilbard Lagho alisema kuwa waumini 12 wanaume walioshwa miguu kuonyesha unyenyekevu ambao Yesu aliagiza waumini kuutimiza.

Padre Lagho aliwasisitiza Wakenya wote kwa jumla kuwa na unyenyekevu na kushirikiana kwa pamoja ili kudumisha uiano na utangamano sambamba na kuliombea taifa hili kuzidi kudumisha amani.

"Wakatoliki huadhimisha siku hii ya Alhamis Kuu kuonyesha unyenyekevu ambao Yesu Kristu alikuwa nao. Hiyo ndiyo sababu tumetekeleza mwongozo ambao Yesu aliutoa kwa kuosha wanaume 12 miguu. Siku hii inafuatiwa na ile ya Ijumaa Kuu ambayo tunaadhimisha mateso ambayo Yesu Kristu alipitia,” alisema Padri Lagho.

Siku ya Alhamis Kuu inafuatwa na Siku ya Ijumaa kuu ambapo Yesu hupitia mateso kisha kusulubiwa. Baada ya siku tatu, waumini huadhimisha sherehe za Pasaka kusherehekea kufufuka kwa Yesu.