Wakazi wa Bahati wametaja unyakuzi wa ardhi ya umma katika eneo hilo kama kikwazo kikubwa cha maendeleo.
Wakizungumza siku ya Ijumaa kwenye mkutano wa majadiliano kati ya wananchi na viongozi wa eneo hilo, akiwemo mbunge Kimani Ngunjiri, wakazi hao walimtaka mbunge huyo kushirikiana na wawakilishi wadi kurejesha ardhi za umma zilizonyakuliwa kwa minajili ya maendeleo.
John Kamau, kutoka wadi ya Dundori, alisema kwamba imekuwa vigumu kuuza ploti katika wadi hiyo, kwani utawala wa kaunti umefunga uuzaji huo kutokana na unyakuzi wa ardhi, huku ploti moja ikidaiwa kumilikiwa na zaidi ya watu wawili.
Samwel Maina, kutoka wadi ya Kabatini, alisema kwa sasa hawana pahala wanapoweza kuita soko, kwani ardhi iliyotengewa soko ilinyakuliwa na mabwenyenye na kugawa katika ploti ambazo baadaye ziliuziwa watu binafsi.
“Hatuna soko hapa Kabatini na akina mama wanalazimika kuuza mboga na matunda kando ya barabara,” alisema Maina.
Mbunge Ngunjiri, ambaye ni mwanachama wa kamati ya ardhi katika bunge la kitaifa, alisema kwamba amefanikisha kurejeshwa kwa ardhi kadhaa za umma katika eneo lake la uwakilishi, na kwa hivyo wembe utakuwa uo huo.
“Nilihakikisha kuwa Shule ya Lemuko imerudishiwa kiwanja chake, na vile vile hospitali ya hapa Kabatini ikarejeshewa ardhi yake. Nitahakikisha kwamba tutapata uwanja wa soko uliokuwa wa umma. Naomba ushirikiano wa wawakilishi wa wadi,” alisema Ngunjiri.
Akizungumzia swala la unyakuzi wa ardhi ya barabara katika wadi ya Bahati, mwakilishi wa wadi hiyo Peter Nderitu, alisema masoroveya wamo kwenye harakati za kufungua barabara hizo, na kuwataka wananchi kukubali kazi watakayofanya kwa mwongozo wa ramani.
Mkutano huo ulifanyika katika ukumbi wa shule ya upili ya Lemuko, wadi ya kabatini.
Baadhi ya wawakilishi wadi waliohudhuria mkutano huo ni Samwel Kamau wa Kiamaina, Paul Thuo wa Kabatini, Steve Kihara wa Dundori na yule wa wadi ya Lanet Mwangi Ngarama.