Wakazi wa Ekerenyo, wilayani Nyamira Kaskazini, walipata fursa ya kujiunga na wawakilishi wa wadi wa bunge la Kaunti ya Nyamira kwenye uwanja wa Ekerenyo ambapo bunge hilo lilifanyia vikao vyao.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akizungumza katika uwanja huo siku ya Alhamisi, spika wa bunge la kaunti ya Nyamira Joash Nyamoko alisema kuwa walianza mpango wa Bunge Mashinani ili kuhakikisha kuwa wananchi wanaelewa kazi ya wawakilishi wao.

Nyamoko alisema kuwa mpango huo utawawezesha wananchi kuelewa jinsi bunge linavyotekeleza vikao vyao na pia watapata fursa ya kuuliza maswali mbalimbali na kujibiwa.

"Baadhi ya wananchi hawapati fursa ya kufika kwenye bunge la kaunti lililoko mjini Nyamira. Mpango huu wa bunge mashinani utakuwa wa manufaa kwao na sisi kwa sababu tutaelewa mahitaji yao na kuyapa kipaombele," alisema Nyamoko.

Nyamoko alisema kuwa mpango huo wa bunge mashinani utakuwa ukifanyika kila wiki na utendelezwa katika sehemu zote za kaunti hiyo.

"Kila wiki wawakilishi watajumuika na wananchi na hiyo itakuwa njia mojawapo ya kuwaleta wananchi pamoja na bunge. Tutahakikisha kuwa tumefika kila sehemu katika kaunti hii,” alisema Nyamoko.