Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Shughuli za usafiri kwenye barabara ya Ikonge-Chabera zilisitishwa kwa muda siku ya Jumapili baada ya wakazi kuandamana kulalamikia huduma duni zinazotolewa na serikali ya Kaunti ya Nyamira.

Wakazi hao walifanya maandamano kulalamikia barabara duni na ukosefu wa usalama unaochangiwa na ukosefu wa taa za mtaani.

Walisema kuwa serikali ya kaunti haipaswi kuendelea kuchukua kodi kutoka kwa wakazi bila kuwapa huduma muhimu.

Wakazi hao waliipa serikali ya kaunti hiyo makataa ya siku 14 kushughulikia matatizo yao kabla ya kukaidi kulipa ushuru.

Waandamanaji hao walioungwa mkono na shirika moja la kijamii kutoka walitishia kuacha kulipa ushuru wakisema kuwa sharti wapokezwe huduma muhimu ikiwa serikali ya kaunti inatarajia wenyeji wa eneo hilo kuendelea kulipa ushuru.

"Tunastahili kupokea huduma muhimu kutoka kwa serikali ya kaunti na tumeipa makataa ya wiki mbili kushughulikia matakwa yetu. Iwapo hilo halitatekelezwa, tutaacha kulipa ushuru," alisema mwanachama wa shirika la Ikonge Civil society Abel Momanyi.

Kwa upande wake, katibu wa uajiri kwenye kaunti ya Nyamira Erick Onchana, aliwahimiza wakazi wa eneo hilo kuwa watulivu kwa kuwa serikali ya kaunti hiyo imeweka mikakati ya kuhakikisha kuwa matakwa yao yanaangaziwa.

"Kaunti hii ni kubwa sana na sharti tuwashughulikie wananchi wote bila ubaguzi. Ninawaomba wananchi kuwa watulivu wanapoendelea kungoja tuwahudumie kwa kuwa tuna mipango yakuezeka taa za solar katika kila eneo Nyamira,” alisema Onchana.