Kamishna wa Nyamira amesema kuwa ili kukabilina na visa vya ukosefu wa usalama, sharti wakazi wawe tayari kushirikiana na maafisa wa usalama.
Akizungumza katika eneo la Kebirigo siku ya Alhamisi, Kamishna Josphine Onunga aliwasihi wakazi kushirikiana na vyombo vya usalama ili kuhakikisha kuwa usalama umeimarika.
Onunga aidha alikanusha madai ya kuzembea kwake latika kudhibiti visa vya ukosefu wa usalama akiongezea kuwa ukosefu wa usalama ni changamoto kuu kote nchini na wala sio Nyamira pekee.
"Swala la usalama linahitaji kila mwananchi kulishughulikia. Sio serikali pekee inayo uwezo wa kuimarisha usalama na ndio maana nawaomba wananchi kuwajibikia usalama wao. Ni makosa kwa mwananchi kulalama kuwa serikali haitekelezi utendakazi wake ilhali mwananchi huyo hasaidii kwa lolote kukabili changamoto ya ukosefu wa usalama," alisema Onunga.
Kamishna huyo aidha alisema kuwa maafisa wa utawala watatumwa katika eneo hilo kusaidia kukabili visa vya ukosefu wa usalama vinavyozidi kuongezeka, huku akiongezea kuwa serikali imejitolea kuhakikisha kuwa mpango wa Nyumba kumi unafanikiwa.
"Tayari nimemwagiza kamanda wa polisi kuhakikisha kuwa maafisa wa polisi wa kutosha wametumwa katika eneo hili il kusaidia kudhibiti visa vya ukosefu wa usalama kwenye vituo mbalimbali. Serikali imejitolea kuimarisha usalama wa wananchi kupitia Nyumba Kumi na inafaa wananchi wajitolee kuhakikisha kuwa hilo linafanikiwa," alisema Onunga.