Share news tips with us here at Hivisasa

Mwakilishi wa wadi ya Kihingo, Kaunti ya Nakuru Stephen Kiarie, amewataka wakazi wa wadi hiyo kushirikiana naye katika vita dhidi ya pombe haramu.

Kiarie alisema hatua hiyo itazuia vifo vinavyoshuhudiwa vhaswa vya vijana.

Akiongea na Radio Amani siku ya Jumatatu, Kiarie alisema kuwa kupitia ushirikiano huo, uuzaji wa pombe hiyo haramu ambayo imekuwa tatizo sugu katika eneo hilo la Kihingo utatupwa katika kaburi la sahau.

Kulingana naye, swala hilo la pombe limekuwa donda ndugu kwani mtu mmoja au hata wawili huaga dunia kila wiki baada ya kubugia pombe hiyo.

“Nataka kuwaomba watu wa Kihingo tupigane na pombe haramu kabisa kwa sababu vijana wetu wanaangamia. Takriban kila wiki tunazika kijana. Ni hasara kubwa sana mwanamume mchanga akiaga dunia. Nawahimiza wazazi tushikane sisi sote ili tuhakikishe hii pombe imemalizwa,” alisema Kiare.

Wakati huo huo, mwakilishi huyo wa wadi alisema kuwa changamoto kubwa katika vita dhidi ya pombe haramu ni ufisadi unaendelezwa na baadhi ya machifu na manaibu wao.

“Ukabilianaji wa pombe haramu kwa wadi hii yangu ni changamoto kubwa kwa kuwa watu wanaohusika ni machifu na manaibu wao. Baadhi yao kwa nyakati zingine wamekuwa wakichukua hongo,” alisema Kiarie.

Haya yanajiri huku dalili za kurejelewa kwa biashara hiyo zikijitokeza baada ya kampeni ya hivi maajuzi ya kumwaga pombe haramu iliyoagizwa na Rais Uhuru Kenyatta kukamilishwa.