Daktari mkuu katika Hospitali ya Rufaa ya Kisii Geofrey Ontomu amesema maafisa wa afya wa kaunti hiyo wataandikisha watu katika kaunti nzima ili kukabidhiwa neti za kujikinga kutokana na ugonjwa wa maleria.
Hii ni baada ya kubainika kuwa maabukizi ya ugonjwa wa maleria yamekuwa kwa kiwangio cha juu zaidi kwa takribani miezi minne sasa.
Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumatano katika hospitali hiyo iliyoko mjini Kisii, Ontomu alisema kuwa hospitali zote za kaunti nzima ya Kisii kufikia sasa zimerekodi asilimia 50% ya wagonjwa ambao wameathirika na ugonjwa wa maleria.
Daktari huyo alisema kuwa eneo bunge la Kitutu Chache Kusini, Bochari na Mugirango Kusini ndio maeneo yaliyorekodi maambukizi ya juu zaidi ikilinganishwa na sehemu zingine za kaunti hiyo.
“Naomba kila mtu ahakikishe amejiandikisha ili kukabidhiwa neti na kujikinga kutokana na ugonjwa wa maleria,” alisema Ontomu.
Aliongezea, “Mutakapopata neti muhakikishe munazitumia inavyostahili maana inasemekana kuwa ugonjwa wa maleria unaweza kusababisha maafa kwa binadamu.”
Aidha, daktari huyo aliongezea kuwa ugonjwa wa maleria kulingana na uchunguzi umeathiri akina mama wajawazito na watoto kwa asilimia kubwa zaidi katika Kaunti ya Kisii.
Anayesimamia Idara ya Afya katika Kaunti ya Kisii Sarah Omache aliomba kila mtu kutumia neti ambayo serikali ya kaunti hiyo inaenda kukabidhi wakazi wa kaunti hiyo.