Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Huku jamii mbali mbali zinazoishi katika kaunti ya Kisii zikijihusisha kwenye masuala ya kilimo mseto, wafugaji na wakulima wa kaunti hiyo wameshauriwa kuanza kutilia maanani kilimo cha kuku wa kienyeji ili kuongeza mapato yao.

Akiongea siku ya Jumatatu katika mji wa Kisii, afisa wa Idara ya kilimo na Ufugaji wa Wanyama Bwana Ignitius Muteshi alisema kuwa wakazi wengi kutoka kaunti ya Kisii wameacha kufuga kuku wa kiasili na kurudia ufugaji wa kuku wa gredi.

Muteshi alisema kuwa kuku hao wa kiasili huwa na faida kubwa ikilinganishwa na wale wengine wa gredi.

“Kuku wa kiasili huwa rahisi kufuga kwa sababu hawali vyakula vya bei ghali kama ilivyo kwenye kuku wa gredi. Vijana ambao hawana kazi wanapaswa kuanza ufugaji huu ili kujiinua kiuchumi kama njia mojawapo ya kujitafutia kazi,” alisema Muteshi.

Muteshi aliwashauri wafugaji kujikita katika kuku hao ambao alisema mayai yao yamekuwa yakihitajika sana na watu kutoka miji mikuu kama vile Nairobi na Mombasa huku akidokeza kuwa mayai ya kuku wa kiasili huwa na virutubisho spesheli ambavyo huwa na umuhimu mkubwa katika afya ya miili ya wanadamu.

Aliwashauri wakulima kutafuta ushauri kutoka kwa wataalamu iwapo watakuwa na moyo wa kuwafuga kuku hao ambayo afisa huyo alisema wako katika hatari ya kupungua katika maboma mengi nchini.