Share news tips with us here at Hivisasa

Wakazi wa kaunti ya Kisii wana kila sababu ya kutabasamu baada ya kampuni ya umeme nchini Kenya Power and Lighting Company (KPLC) kuweka mikakati ya kuanza kutoa mafunzo kuhusu jinsi ya kujikinga kutokana na hathari za nguvu za umeme.

Akizungumza siku ya Jumatatu na waandishi wa habari mjini Kisii, meneja wa kampuni ya KPLC mkoani Nyanza, Chris Omwenga, alisema kampuni hiyo itaanza kutoa mafunzo kwa wakazi wa Kisii ya jinsi ya kuepuka kupigwa na nguvu za umeme.

Hii ni baada ya watu wawili kuaga dunia katika katika eneo la Kiogoro na mjini Kisii kwa muda wa majuma matatu kufuatia kupigwa na nguvu za umeme.

Omwega alisema kuwa waliamua kutoa mafunzo hayo ili wakazi wa Kisii wasiwe wanapoteza maisha kila wakati kutokana na kupigwa na nguvu za umeme.

“Kampuni ya KPLC ikishirikiana na serikali ya kaunti ya Kisii itatoa mafunzo kwa wakazi wa Kisii. Tayari mikakati ya kuanza kuwafundisha watu kuhusu hatari za umeme na jinsi mtu anastahili kuepuka kupigwa na nguvu hizo imeisha. Lile ambalo tumebakisha ni kuchagua siku ya kuanza kufanya mafunzo hayo, ambayo yanatarajiwa kuanza juma lijalo,” alisema Omwenga.

Aidha, meneja huyo aliwaonya wakazi dhidi ya kukaribia nyaya za umeme zilizoanguka kwani itakuwa hatari kwao.

Alisema kuwa wakazi wanapoona nyaya zilizokatika, wanapaswa kuripoti visa hivyo kwa kampuni hiyo ili nyaya hizo zirekebishwe.