Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Huku wakazi wa Mombasa wakisubiri kutekelezwa kwa mradi wa kuimarishwa kwa bwawa la maji la Mwache, katika kaunti ya kwale, wakazi wa Migombani, Likoni, wamesalia kutumia maji ya kisima kutokana na uhaba uliopo wa maji safi.

Wakizungumza siku ya Jumatano, wakazi wa eneo hilo wakiongozwa na Abdallah Juma, walidokeza kuwa uhaba huo wa maji safi katika eneo hilo umepelekea wakazi kutembea kwa masafa marefu kutafuta bidhaa hiyo muhimu.

Wengi wanaoishi katika maeneo hayo ya Likoni walisema kuwa uhaba huo wa maji safi umewafanya wauza maji kupandisha bei ya bidhaa hiyo, ambayo kwa sasa imeonekana kuwalemea wakazi kutokana na hali ngumu ya kimaisha na kuongezeka kwa mahitaji yao ya kila siku.

Juma alilezea harakati ngumu anazokumbana nazo kila uchao kwa kutembea kwa kilomita kadhaa kabla ya kupata maji safi yakutumika kwa mapishi na kunywa.

“Maji safi yamekuwa shida kupata na bei yake imepanda mpaka twashindwa tuelekee wapi ili kuepukana na matatizo haya,” alisema Juma.

Baadhi ya wakazi katika maeneo hayo wameonekana kutafuta mbinu mbadala ya kutumia maji ya kisima ambayo wengi wao wamedai kuwa yana kiwango kikubwa cha chumvi, ikizingatiwa ukaribu wa maeneo yao na Bahari Hindi.

Wakazi wengine walidai kuwa maji hayo ya kisima yamechangia katika kuleta baadhi ya maradhi hasaa ya tumbo.

Hata hivyo wakazi hao wameitaka serikali ya kaunti ya Mombasa kuchukua hatua za haraka katika kufanikisha mradi huo wa ujenzi wa bwawa la Mwache ili maji safi yaweze kupatikana kwa wingi na kwa urahisi.