Wakazi wa Mariakani wamezitaka serikali za kaunti ya kuingilia kati namna raslimali za kaunti zinavyotumika kwenye miradi mbalimbali iliyoanzishwa chini ya serikali ya ugatuzi.
Wakazi hao wamesema kuwa mji kama wa Mariakani unaopatikana katika barabara kuu ya Mombasa-Nairobi na unaokuwa kwa kasi sasa unakumbwa na hatari ya kutokuwa na namna ya kukabili visa vya dharura kwa kile wanachokitaja kama kutokuwa na miundo msingi ya kukabili visa vya dharura katika eneo hilo.
Kulingana na Ali Chiro ambaye ni mkaazi wa eneo la Njoro Takatifu, tangia upanuzi wa barabara kuu ya kuelekea jijini Nairobi uanze hadi sasa wakazi wamekuwa wakikumbwa na shida nyingi ikiwemo mabomba ya kusafirishia maji taka kutoka kwa makazi yao kuvunjwa huku wakisema kuwa huenda wakaathrika kutokana na mvua kubwa zinazotarajiwa kunyesha kwenye msimu huu wa mvua za masika kauli ambayo iliungwa mkono na Hussein Mwikali ambaye ni mfanyabiashara katika soko la Mariakani.
Wakitoa mfano wa hivi majuzi ambapo serikali ya kaunti ya Kilifi ilitoa magari ya zima moto na hata kutoa fedha za uwezo fund kwa vijana wa eneo hilo, wakazi hao wamesema kuwa kwa sasa magari hayo hayajaonekana kusaidia kwani visa vingi vya nyumba kuteketea vimeripotiwa eneo hilo ila hakna hata mkasa mmoja ambapo gari la kukabili janga la moto lilionekana.
Aidha wameongeza kuwa kiasi hicho cha fedha kilichotolewa na mbunge wa Kaloleni Gunga Mwinga chini ya mradi wa Uwezo fund hazijaonekana kuwafaidi.