Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Kuongezeka kwa idadi ya watu mjini Nakuru kumesababisha kupanda kwa gharama ya maisha mjini humo.

Wakaazi wanashuhudia uhaba wa nyumba za kupangisha kwenye mitaa mbali mbali. Hali hii imefanya kodi za nyumba kupandishwa maradufu katika mitaa mingi.

Kulingana na utafiti uliofanywa na mwandishi huyu katika mitaa ya Maili Sita na Zanzibar, kodi imepanda kwa takriban asilimia 50 ama 100.

Wakaazi katika mtaa wa Maili Sita wanasema nyumba iliyokuwa ikilipishwa shilingi elfu moja miaka miwili iliyopita sasa inalipishwa shilingi elfu moja mia tano hadi elfu mbili.

Kulingana na James Mwaniki ambaye ni mmiliki wa nyumba mtaani Zanzibar, ukosefu wa nyumba za kutosha na kupanda kwa gharama ya maisha ni baadhi ya mambo yanayofanya kodi kupanda.

“Miaka michache iliyopita ilikuwa rahisi sana kupata nyumba ya bei nafuu mjini Nakuru lakini kutokana na kuendelea kuongezeka kwa watu tumeshuhudia kupanda kwa gharama ya kodi na pia ukosefu wa nyumba za kutosheleza mahitaji,” Mwaniki alisema.

Katika mtaa wa Zanzibar wanaotafuta nyumba za kupangisha wanalazimika kuwalipa maajenti kati ya shilingi elfu moja na elfu mbili ili kuwatafutia nyumba.

“Kama hutaki kusumbuka ukitafuta nyumba utalazimika kumlipa ajenti ili akusaidie kutafuta nyumba na hii inaumiza mpangaji kwa sababu bado atalazimika kulipa kodi ya nyumba na mambo mengine,” Alice Mwenje, mpangaji mjini humo, alisema.