Wakazi wa eneo la Mokomoni wilayani Borabu kaunti ya Nyamira wamelalamikia ongezeko la visa vya kuvamiwa katika eneo hilo kila wakati na kuomba maafisa wa polisi kuwasaidia .
Hii ni baada ya washukiwa wa ujambazi kuvamia wakazi wa eneo hilo usiku wa kuamkia Jumatatu, huku wawili wakijeruhiwa na kupelekwa katika hospitali ya Tenwek kwa matibabu zaidi.
Wakizungumza siku ya Jumapili katika eneo hilo la Mokomoni, wakazi hao wakiongozwa na Peterson Onsase walisema wamekuwa wakivamiwa kila wakati na kuomba usaidizi kutoka kwa serikali kupitia maafisa wa polisi.
“Kila wakati tunasumbuliwa na kuteswa kupitia washukiwa wa ujambazi hapa Mokomoni, na katika kaunti ya Nyamira kwa ujumla, sasa tutafanya nini? tunaomba maafisa wa polisi kutuwekea usalama wetu,” alisema Onsase.
“Ikiwa serikali inahitaji kutusaidia, huu ndio wakati tunaomba usalama kuimarishwa kabla hatujauliwa tuishe katika eneo hili,” alisema Ogari Mose, mkazi mwingine.
Katika kaunti ya Nyamira, visa vya uvamizi vimekuwa vikiripotiwa kila kuchao, na ahadi za usalama zikitolewa kila wakati ambazo hazina manufaa hayo ni kwa mujibu wa wakazi hao ambao wanaomba usalama.