Shughuli za usafiri zilisitishwa kwenye barabara ya Molo kwenda Olenguruone baada ya wakaazi wa Moto kuandamana asubuhi Jumapili kulalamikia ongezeko la pombe haramu.
Hii ilijiri baada ya mwanamume wa umri wa makamo kupatikana akiwa amefariki kando ya barabara asubuhi ya Jumapili baada ya kusemekana kuwa alikunywa pombe haramu usiku wa Jumamosi.
Kulingana na wakaazi hao, uuzaji wa pombe haramu umerudi kwenye mtaa huo miezi kadhaa baada ya pombe hio kumalizwa.
"Tumetoa tetesi kuhusu kuuzwa kwa pombe hii lakini chifu wa eneo hili amepuuza," alisema Robert Muturi.
"Mzee huyu alikunywa pombe jana na tunadhani baada ya mvua kunyesha, alishindwa kutembea na kuanguka vibaya, " aliongeza Hezron Kuria.
Wakazi hao waliapa kuandamana hadi hatua ichukuliwe kuwafurusha wanaouza pombe hiyo.