Wakazi wa eneo bunge la Kisauni wameshauriwa kuzingatia umuhimu wa nyumba kumi ili kuwatambua wageni wanaoingia katika maeneo yao kama njia moja wapo ya kukabuliana na kukithiri kwa visa vya uhalifu.

Share news tips with us here at Hivisasa

Kulingana na Kiongozi wa vijana katika eneo hilo Maxwell Masai, kukithiri kwa visa vya uhalifuu katika eneo hilo kumechangiwa na wakazi wenyewe kutotilia maanani umuhimu wa nyumba kumi huku akisema kuwa iwapo wakazi watalizingatia swala hilo basi uhalifu Kisauni utapungua.

Akizungumza katika eneo la Mtopanga huko Kisauni mjini Mombasa siku ya Jumatano, Masai amesema kuwa kuna haja ya jamii kuhamasishwa zaidi kuhusu umuhimu wa ubalozi wa nyumba kumi na kuhakikisha kuwa kila mgeni anayeingia katika eneo hilo anasajiliwa kwa afisi za mabalozi wa nyumba kumi.

Amesema kuwa wazee na vijana wa eneo hilo wameahidi kushirikiana na maafisa wa usalama kuhakikisha kuwa eneo bunge la Kisauni hasa maeneo ya Mtopanga, Bumburi, Mshomoroni, Mwandoni, Mlaleo na Barsheba yanapewa usalama zaidi kwani ndio maeneo ambayo vijana wengi hufanya uhalifu.

"Tunawaomba wakaazi kushirikiana na maafisa wa usalama katika kuimarisha usalama wa eneo hili ili kuhakikisha kuwa visa vya kihalifu vinasitishwa na vijana waliyojitosa katika uhalifu wanashauri na kujitenga na uovu huo," alisema Masai.

Kiongozi huyo wa vijana ameahidi kuandaa vikao vya hamasa wa wakaazi wa eneo hilo kuhakikisha kuwa swala ya nyumba kumi inatiliwa mkazo zaidi ili usalama kuimarishwa.