Kufuatia idadi kubwa ya wakazi wa Mombasa kukosa vyeti vya kuzaliwa, sasa wakazi hao wajitokeza kwa wingi na kuukumbatia mpango huo uliozinduliwa kwa minajili ya kuwasaidia wakazi hao kutimiza malengo yao.
Mpango huo uliozinduliwa na mfanyibiashara mkubwa katika eneo la Kisauni Ali Mbogo siku ya Alhamisi na kutarajiwa kuendelea hadi siku ya Jumapili, idadi kubwa ya wakazi wa eneo hilo ilibainika kuwa hawana vyeti hivyo.
Akizungumza na wanahabari kwenye kituo hicho kichoandaliwa Mtopanga eneo bunge la Kisauni siku ya Alhamisi, Mbogo alisema kuwa kutokana na serikali pamoja na mbunge wa eneo hilo Rashid Bedzimba kukosa kuwasaidia wakazi wa eneo hilo kumechangia wakazi hao kurudi nyumba kimaendeleo.
Mbogo alishikilia kuwa atahakikisha wakazi wa eneo hilo wamefaidika katika maswala tofauti ya kimaendeleo ikiwemo huduma bora za matibabu, elimu, muundo msingi na uimarishaji usalama kwani maswala hayo ndio yanayowakandamiza wakazi wa eneo hilo.
“Tumeamua wakati huu kuwaunganisha wakazi wa eneo bunge la Kisauni kuwasaidia kutimiza malengo yao hasa hasa kuwa na afya bora, elimu, barabara na usalama kwa sababu eneo hilo bado linapitia changamoto licha ya kuwa na kiongozi kwa muda wa miaka mitatu bado hajawafanyia wakazi mambo muhimu,” alisema Mbogo.
Wakati huo huo, alitangaza kuwania kiti cha ubunge wa Kisauni na akawarai wakazi kuhakikisha kuwa wanamchagua kama kiongozi wao pindi uchaguzi mkuu utakapowadia.
Mfanyibiashara katika eneo la Kisauni Ali Mbogo akiwasaidia wakaazi kujaza fomu za kupata vyeti vya kuzaliwa katika eneo la Mtopanga eneo bunge la Kisauni.
Cheti cha kuzaliwa. Wakazi wa Mombasa walijitokeza kwa idadi kubwa ili kujisajili kupokea vyeti hivyo.