Share news tips with us here at Hivisasa

Shirika la Msalaba Mwekundu tawi la Nakuru limewahimiza wakazi kujitolea kutoa huduma zao kwa shirika hilo.

Akizungumza siku ya Alhamisi katika hoteli ya Legacy mjini Nakuru, kwenye shughuli ya kutoa mafunzo kwa wanahabari kuhusiana na jinsi shirika hilo linavyotekeleza majukumu yake, Mwenyekiti wa shirika hilo katika Kaunti ya Nakuru, Dkt Njeri Muhia alisema kuna njia nyingi ambazo wakazi wa Nakuru na Wakenya kwa jumla wanaweza kujitolea kutoa huduma zao kwa shirika hilo kama vile kupitia kwa uandishi wa habari kuhusiana na shirika hilo.

Alisema kuna takriban watu 2,000 waliojitolea kutoa huduma zao kwa shirika hilo mjini Nakuru, idadi ambayo aliashiria kuwa ni ndogo mno ikilinganishwa na ile ambayo wanalenga.

“Wanaojitolea kutoa huduma zao kwa shirika hili la Msalaba Mwekundu sio wale tu wanaotumika kuwasaidia wanaokumbwa namajanga au ajali. Wanahabari pia wanaweza kujitolea kwa kutoa taarifa kwa Wakenya kuhusiana na shirika hili na pia kwa kutoa taarifa za majanga au ajali zilizotokea ili tuweza kuwasaidia waathiriwa,” alisema Dkt Muhia.

Kwa upande wake, Jonuba Bekah, mmoja wa waliokuwa wakitoa mafunzo hayo alisema kwamba kuna mambo mbalimbali yanayochangia kwa uwepo wa idadi ndogo au kubwa ya wanaojitolea kutoa huduma zao kwa shirika hilo katika maeneo mbalimbali.

Mojawapo ya sababu hizo kwa muujibu wake ni kwamba wengi wa wanaojitolea kutoa huduma zao kwa shirika hilo ni vijana ambao hujitolea kwa muda mfupi na kisha huanza shughuli zingine hapo baadaye kama vile kuelekea katika miji mingine kwa shughuli za kimasomo.

'Wengi wanaojitokeza kutoa huduma zao kwa Shirika la Msalama Mwekundu ni vijana ambao hufanya mambo mengine baada ya muda mfupi. Isitoshe, kulingana na sheria, mtu hawezi kujitolea kutoa huduma zake kwa shirika fulani kwa zaidi ya siku tisini bila ya mtu huyo kupewa ajira ya kuhudumu,” alisema Bekah.