Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Wakazi kutoka Kaunti ya Nakuru wameshtumu kile walichokitaja kama hatua ya baadhi ya viongozi kuyatumia makundi haramu kusambaratisha maandamano ambayo yamepangwa na wananchi na yanayolenga kuwakosoa.

Wakiongea na wanahabari mjini Nakuru siku ya Ijumaa, wakiongozwa na aliyekuwa mwenyekiti wa chama cha TNA katika Kaunti ya Nakuru Dkt Abdul Noor, wakaazi hao walimtaka OCPD wa Nakuru kuchunguza waliohusika katika kuwafadhili vijana waliosambaratisha maandamao yao siku ya Alhamisi.

Wakazi hao walitaja hatua hiyo kama ya kuwakandamiza wakazi katika kaunti ya Nakuru na kusema kuwa wana uhuru wa kuelezea lalama zao kwa njia ya amani na haki.

“Tulikumbana na genge la watu ambalo tunashuku ni mojapawapo ya makundi haramu na waliweza kutuvaia na kumteka kijana mmoja nyara kwa zaidi ya masaa matatu. Hiyo ilikuwa njia moja ambayo imetumiwa na baadhi ya viongozi kwenye Kaunti ya Nakuru kuhakikisha wametuzuia kuwasilisha makaratasi yetu ya kulalamikia utumizi mbaya wa fedha kwa tume ya kukabiliana na ufisadi ya EACC,” alisema Dkt Noor.

Wakazi hao walisema kijana huyo, John Njoroge, ataandikisha ripoti katika kituo cha upelelezi ili uchunguzi mwafaka uweze kufanyika na sheria kuchukuliwa dhidi ya waliohusika katika kupanga njama hiyo.

Kwa upande wake, Njoroge alisema kuwa kamwe hawatakoma kuitoa lalama endapo kutakuwa na hitaji hilo.

Kaimu OCPD wa Nakuru Musa Kongoli aliahidi kwamba uchunguzi utaendelezwa kuhusiana na madai hayo ili hatua mwafaka za kisheria zichukuliwe.