Kufuatia athari zilizotolewa kuhusu mvua ya El Nino nchini, Gavana wa kaunti ya Nyamira John Nyagarama amejitokeza kuwasihi wananchi kujitayarisha kwa mvua hiyo.
Akiwahutubia wanahabari siku ya Jumapili, Nyagarama alisema kuwa kuanza kunyesha kwa mvua hiyo huenda kukasababisha hasara kubwa
Aliwaomba wakazi kuwa macho kuepukana na hatari ambazo huenda zikasababishwa na mvua hiyo.
"Mvua ya El Nino ambayo imeanza kunyesha katika sehemu zingine nchini huenda ikasababisha mafuriko makubwa, uharibifu wa mimea na hata pia vifo. Nawasihi wakazi wa Nyamira kuwa macho kuepukana hatari zinazoletwa na mvua hiyo,” alisema Nyagarama.
Akizungumzia swala lakujiandaa kukabiliana na mvua hiyo, Nyagarama alisema kuwa serikali yake imeanza kukarabati barabara mbalimbali za kaunti hiyo kwa kutumia tinga tinga mpya zilizonunuliwa na pia ameziomba kampuni za kibinafsi hasa za chai kufungua mitaro na mabomba yaliyoziba ili yasije yakaleta magonjwa.
Nyagarama amewaomba wakazi wanaoishi kwenye nyanda za chini hasa wale wa eneo bunge la Borabu na Mugirango Kaskazini kuhamia nyanda za juu kwa usalama wao huku akiwasihi wazazi kuwalinda wanao dhidi yakucheza kando kando mwa timbo za maji.