Hatua ya kusimamishwa kazi kwa mkurugenzi mkuu wa shirika la mafuta nchini National Oil Corporation imezua hisia kali kutoka kwa baadhi ya wakazi wa eneo la Pwani.
Baadhi ya wakazi walisema kuwa hatua hiyo huenda ikaendelea kuwatenga wakazi wa maeneo husika kukosa kuipigia kura serikali.
Wakiongea na mwandishi huyu katika jiji la Mombasa siku ya Alhamisi, wakazi hao walisema kuwa kusimamishwa kazi kwa Sumayya Athman huenda kukapoteza baadhi ya wafuasi ambao tayari walikuwa wameanza kuunga mkono upande wa serikali, baada ya ziara ya Rais Uhuru Kenyatta mwezi jana.
Wakiongozwa na Tim Charo, wakazi hao walisema kuwa waziri mpya wa Kawi amechukua hatua ambayo itaathiri msimamo na mtazamo mzima wa wakazi ambao wanaitaja hatua hiyo kuwa ya kisiasa.
Walisema kuwa hatua hiyo haifai kamwe kwa wakati huu ambao serikali ya Jubilee inataka kurudishwa mamlakani kufika mwaka ujao.
“Hatua kama hii ya kusimamisha Bi Sumayya kazi ina mwelekeo mbaya wa siasa na inalenga kuwanyamazisha wakazi na kuwanyima wenyeji nafasi ya kuwa na kazi za serikali kama wengine,” alisema Charo.
Aliwataka viongozi wakuu wa Jubilee kuliangalia suala hilo kwa umakini.
Bi Sumayya anatoka kwenye eneo bunge la Malindi na hatua ya kupewa likizo ya lazima na waziri imetajwa kuwa inayoweza punguza imani ya wakazi wa Malindi ambao wanatarajia kupiga kura kwenye eneo bunge hilo mwezi ujao.
Baadhi ya wachanganuzi wa siasa wamesema kuwa huenda kiti hicho kikashindwa na upinzani.