Wakazi wanaoishi maeneo ya mabonde wametakiwa kuwa waangalifu na kuyahama maeneo hayo ili kuepukana na majanga wakati wa mvua ya El Nino.
Kulingana na Gavana wa kaunti ya Tana River, Hussein Dado, huenda mvua hiyo ikasababisha madhara makubwa kwa wakazi endapo tahadhari hiyo haitazingatiwa.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumatano katika halfa ya harambee, Dado alisema kwamba serikali za kaunti zimejiandaa kikamilifu kukabiliana na majanga endapo yatashughudiwa.
Dado amesema kwamba wakazi wanaoishi karibu na mito wanafaa kuyahama maeneo hayo ambayo hushuhudia mafuriko na maporomoko.
“Tungependa kuwatahadharisha wakazi kuhusu mvua ya El Nino ambayo inatarajiwa kunyesha. Wakazi wanapaswa wayahame maeneo hayo na kuishi sehemu za ukame ili kuepuka mikasa,” alisema Dado.
Aidha, alisema kuwa serikali za kaunti zitahakikisha kuwa waathiriwa wanapata hifadhi katika maeneo mazuri kwani mikakati mwafaka imeidhinishwa ili kuona kwamba wakazi hawaathiriki na mikasa inapotokea.
“Kama viongozi wa kaunti tuko tayari kuhakikisha kuwa wakazi hawathiriki na mikasa kama tulivyoshuhudia miaka iliyopita kwani serikali kuu na zile za kauniti zinashirikiana katika kuhakisha kuwa wananchi wako salama,” aliongezea Dado.
Mvua hiyo ya El Nino ilitangazwa na idara ya utabiri wa hali ya anga nchini kuwa itanyesha kwa zaidi ya miezi mitatu kuanzia mwezi wa Octoba.