Wakaazi wa eneo la Barut viungani mwa mji wa Nakuru, wamepongeza maafisa wa utawala wa mkoa katika kata hiyo kwa kukabiliana na unywaji na ugemaji wa pombe haramu.

Share news tips with us here at Hivisasa

Wakizungumza siku ya Jumanne, wakaazi hao kupitia Miriam Cherotich, walisema kwa siku za hivi karibuni, utawala wa mkoa katika eneo hilo umekuwa ukikabiliana na bidhaa hiyo haramu huku baadhi ya wagemaji wakionekana kukumbatia kilimo baada ya vita hivyo kuchacha.

Aidha wametaka maafisa hao kuzidisha msako wa mara kwa mara katika kingo za mto Ndarugo ambako wanadai ni handaki kuu ya upishi wa pombe hiyo, ili kuhakikisha bidhaa hiyo inamalizwa kabisa.

“Tunawahimiza maafisa wa polisi na wa utawala wa kimikoa waendeleze kabisa vita vya pombe ili kuhakikisha kuwa imemalizwa kabisa, wasilegeze kamba maanake wanafanya jambo zuri,” Cherotich alisema.

Vile vile wamependekeza utawala wa mkoa, maafisa wa polisi na wazee wa nyumba kumi kubuni uhusiano mwema wa karibu na wenyeji wa eneo hilo ili waweze kuwapasha habari muhimu bila kuogopa, zitakazopelekea kunaswa kwa wanaoendeleza biashara hiyo haramu katika eneo hilo.