Mwanasiasa Petterson Mittau wa eneo bunge la Changamwe amewataka viongozi wa eneo hilo kuwa wazi kuhusu uhaba wa maji ambao umewakumba wakaazi wa eneo hilo tangu mwezi Januari mwaka huu.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Mittau amesema kuwa ni wazi mradi ya ujenzi wa barabara ya reli ya kisasa, upanuzi wa bandari ya Mombasa na upanuzi wa barabara ya Changamwe kuelekea katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Moi huko Changamwe imepelekea uhaba huo wa maji.

Mittau amemshinikiza Mbunge wa Changamwe Omar Mwinyi kutafuta mwafaka wa tatizo hilo katika afisi za kampuni ya usambazaji maji mjini Mombasa sambamba na wahusika wakuu wa kampuni za uhandisi kutoka nchini Uchina.

Amehoji kuwa maji waliyokuwa wakisambazwa kwa wakaazi hao sasa yanaelekezwa katika maeneo ambayo miradi hiyo inatekelezwa, huku serikali ya Kaunti ya Mombasa na viongozi waliyo mamlakani wakikosa kuliwajibikia swala hilo.

“Tunamtaka mbunge wa eneo hilo Omar Mwingi kuhakikisha amefanya mazungumza na serikali ya kaunti, wasimamizi wa maji Mombasa ili kuhakikisha kuwa tatizo la uhaba wa maji linatatuliwa,” alisema Mittau siku ya Jumamosi katika eneo la Changamwe.

Kampuni ya usambazaji maji ya Mombasa imepinga madai hayo na kusema kuwa tatizo la maji katika kaunti hiyo limechangiwa na kufungwa kwa kituo cha kusukuma maji cha Baricho ambacho kinafanyiwa marekebisho.