Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wakazi wa Sankuri na viunga vyake wameambiwa kuwachagua viongozi wenye nia ya kuleta maendeleo wakati wa uchaguzi mwaka ujao.

Hayo yalisemwa na mbunge wa Balambala, Abdi Omar alipokuwa ametembelea eneo hilo siku ya Jumapili katika harakati ya kujipigia debe katika kampeni yake ya kutaka kuchaguliwa tena kwenye uchaguzi mkuu ujao. Omar alisema kuwa wananchi wa eneo hilo wamechoka kuwachagua viongozi ambao hawaleti maendeleo kwa watu waliowachagua na azma yao ni tu kujinufaisha kisiasa.

“Mimi nataka kuwaambia nyinyi siku ya leo muwe na makini na watu mnaowachagua kwenye uchaguzi mkuu ujao. Ni haki yenu kuchagua watu wa kuleta maendeleo,’’ alisema Omar.

Omar alitoa wito kwa wakazi wa Sankuri kujisajili kupokea vitambulisho na kadi za kupiga kura kabla ya uchaguzi mkuu ujao.

“Hatua ya kwanza ya utawala mzuri na wenye demokrasia ni kuwa na uwezo wa kuchagua viongozi bora na hii inawezekana tu ikiwa mtapata vitambulisho na kadi za kupiga kura,” alisisitiza Omar.