Wakazi wa Embong'a kata ya Keera katika eneo bunge la Mugirango magharibi wamejitokeza kulalamikia vikali hatua ya kampuni ya usambazaji umeme nchini KPLC tawi la Nyamira kukata nguvu za umeme katika eneo hilo. 

Share news tips with us here at Hivisasa

Kwenye mahojiano na wanahabari siku ya Jumatano baada yao kushiriki  maandamano ya kilomita kumi, wakazi hao walishangazwa na ni kwa nini kampuni hiyo iliwakatia umeme ikizingatiwa kwamba hali hiyo imesambaratisha shughuli katika eneo hilo. 

"Ni kitu cha kushangaza kwamba kampuni ya KPLC inaweza tukatia nguvu za umeme kwa kung'oa transforma moja katika eneo la Bumburi hali ambayo imeathiri usambazaji umeme katika eneo la Bonyunyu, Rionyang'i, Embong'a na Kenyoro, ilhali wanafahamu kuwa shughuli za kibiashara na hasa za afya kwenye hospitali ya Embong'a zinasambaratika," alisema Soranus Bundi. 

Bundi aidha aliongeza kusema kuwa huenda hali hiyo ya wakazi wa eneo hilo kukatiwa nguvu za umeme ikawa inasinikishwa kisiasa kutokana na kukataa kwa wakazi hao transforma moja kuhamishwa kutoka eneo la Bumburia. 

"Hii hatua ya kampuni ya Kenya power kutukatia nguvu za umeme huenda ikawa inasinikishwa kisiasa na  baadhi ya watu wanaotaka kampuni ya Kenya Power kutuhangaisha kwa sababu wakazi wa Bumburia walikataa kuruhusu kampuni ya Kenya power kuiondoa transforma katika eneo hili," aliongezea Bundi. 

Juhudu za kuzungumza na meneja wa kampuni ya usambazaji umeme nchini tawi la Nyamira Dancan Machuka kuhusiana na suala hilo ziliambulia patupu baada yake kukosa kuchukua simu.