Wakaazi wa wadi ya Magenche iliyo katika eneo bunge la Bomachoge Borabu wameiomba serikali kuingilia kati na kutatua mzozo wa mipaka katika sehemu hiyo.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akiongoza kikundi hicho hadi ofisi za kamishina wa kaunti ya Kisii Chege Mwangi mnamo siku ya Alhamisi, Kennedy Marando alisema baadhi ya viongozi kutoka sehemu hiyo wanachangia katika mzozo huo na hivyo kuomba utatuzi wa haraka kufanywa.

“Kuna viongozi ambao wanatumia makundi ya vijana ili kuzua vurugu, tunaiomba serikali kuwachukulia hatua za kisheria. Mipaka ya lokesheni ilitengenezwa kitambo na wazee, kwa hivyo yeyote anyeiingilia anafanya kinyume na sheria,” alihoji Marando.

Kulingana na naibu kamishina wa Kisii Philip Soi, watakaopatikana wakiwachochea wananchi dhidi ya wengine watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Akiongea na walalamishi hao, Soi aliwahakikishia kuwa swala la mipaka litashughulikiwa na kutafuta suluhu la kudumu.

“Kumekuwa mzozo wa mipaka katika koo mbalimbali katika eneo bunge hilo ukiwemo ule kati ya jamii mbili zinazoishi katika mpaka wa kaunti za Kisii na Narok. Tutalishughulikia suala hilo ili kuhakikisha wakaazi wa sehemu hiyo wanaishi kwa Amani,” alionya naibu kamishina.

Soi pia amewaonya vijana dhidi ya kutumiwa na wanasiasa kwa manufaa yao, na badala yake amewasihi kujishughulisha na miradi itakayowanufaisha maishani.