Wakaazi wa Wadi ya Kisii ya Kati katika sehemu ya Kiamabundu na Bitengero Kaunti ya Kisii watanufaika na mradi wa kuchimbiwa visima vya maji katika maeneo hayo.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Akiongea siku ya Alhamisi katika ofisi yake, Mwakilishi wa Wadi hiyo Monyenye Yoge amesema kuwa wakaazi hao watanufaika kutokana na mradi wa kuchimbiwa visima ili wapate maji hasa wakati wa kiangazi.

Monyenye alisema Serikali ya Kaunti ya Kisii imeweka mikakati ya kutenga pesa zitakazo tumika  kwa uchimbaji wa visima katika Wadi mbali mbali huku Wadi yake ikiwa moja ya Wadi hizo.

“Serikali ya Kaunti ina mikakati kabambe ya kuchimba visima katika Wadi mbali mbali nasi kama wakaazi wa Wadi ya Kisii ya Kati tutanufaika pakubwa na mradi hiyo,” alisema Monyenye.

Aidha, aliongezea kuwa kinamama husumbuka sana wakati wa kiangazi kwa kuenda mtoni na kuchukua muda mrefu kufuatia idadi ya watu wengi wanaotegemea maji hayo, lakini visima vivyo vitakavyochimbwa vitawasaidia pakubwa kwa kuwa zitakuwa karibu na makaazi yao.

Kwa upande wa barabara, Mwakilishi Monyenye amesema anaendelea kuhakikisha kuwa barabara katika Wadi hiyo zimekarabatiwa ili kuinua viwango vya maendeleo na uchukuzi katika Wadi hiyo.

Wakaazi hao wamempongeza Mwakilishi Monyenye kwa bidii ya kufungua na kukarabati baadhi ya barabara ambazo hapo mbeleni hazikua zinapitika kama barabara ya Gekomu kuelekea Mwembe na nyinginezo.

“Tunampongeza Mwakilishi Monyenye kwa kulikarabati barabara ya Nyanchwa-Kiamabundu na siku hizi mimi kama mfanyibiashara hufika sokoni mapema bila hata kusumbuliwa na matope kwa kuwa barabara zinapitika kwa njia ya urahisi,” alisema James Matoke mmoja wa wakaazi hao.