Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Madereva wa magari ya uchukuzi wa umma mjini Nakuru na viunga vyake walifanya maandamano Jumatatu kulalamikia tukio la kutoweka kwa viongozi wawili wa sekta ya magari ya uchukuzi wa umma mjini humo.

Wawili hao ambao pia ni wafanyibiashara maarufu mjini Nakuru wanaofahamika kama Joseph Ngugi almaarufu Jose na Simon Wachira almaarufu Shem walitoweka Ijumaa ya tarehe 22 Januari.

Inadaiwa kuwa walikuchukuliwa na jamaa wanaodaiwa kuwa maafisa wa polisi waliokuwa wamejihami katika mtaa wa White House viungani mwa mji wa Nakuru, huku gari linalodaiwa kutumiwa kuwateka nyara likipatikana katika eneo la Kikopey Jumamosi asubuhi.

Mbunge wa eneo bunge la Nakuru mashariki David Gikaria aliyejitokeza kuhutubia kundi hilo alishutumu tendo hilo pamoja na lile la maafisa wa polisi la kukosa kutoa ripoti yoyote kuhusiana na tukio hilo la utekaji nyara.

Aidha, mbunge huyo pia alishutumu tukio la maafisa wa polisi kutumia vitoa machozi dhidi ya waandamanaji hao walioandamana hadi katika kituo cha polisi cha central kilichoko Nakuru.

Wakati huo huo, Gikaria aliitaka idadi ya polisi kuongezwa mjini Nakuru ili usalama wa wananchi uweze kuimarishwa.

Jumamosi iliyopita Simon Chege, nduguye Ngugi alielezea hofu akisema hawajapata mawasiliano kutoka kwa wawili hao, huku akiarifu wanahabari kwamba baada ya kuripoti tukio hilo kwa polisi wa Gilgil, waliarifiwa kuwa simu za rununu za waili hao zilikuwa zimezimwa.