Shughuli za kawaida zilitatizika katika barabara ya Nyamusi-Magwagwa kwenye eneo bunge la Mugirango Kaskazini mapema Ijumaa baada ya wakazi wa eneo hilo kupanda ndizi kwenye barabara hiyo kulalamikia kutopitika kwake. 

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Wakaazi hao walisema waliamua kuchukua hatua hiyo kwa sababu wamekuwa wakipitia changamoto nyingi wakati wa kusafirisha mazao yao sokoni, kufikisha wagonjwa hospitalini na shughuli mbalimbali za kila siku huku wakiongezea kuwa hamna kiongozi yeyote amejitokeza kuwasaidia. 

"Kwa kweli sisi kama wakazi wa eneo hili kwa muda sasa tumekuwa tukilalamikia hali mbaya ya barabara hii, na kwa maana hamna kiongozi yeyote anayejitokeza kutusaidia, ndio maana tumeamua kupanda miti katika barabara hii," alisema mmoja wa mkaazi wa eneo hilo James Marita. 

Wakazi hao aidha wameitaka serikali ya kitaifa kuingilia kati na kutengeneza barabara hiyo ili warejelee shughuli zao za kawaida.

"Ni ombi letu kwa serikali ya kitaifa kuchukua hatua ya kutusaidia kukarabati barabara za eneo hili vyema ili kuturahisishia usafiri," aliongezea Marita.