Mamia ya wakaazi wa Garissa siku ya Jumatatu waliandamana wakidai kuwa serikali haiwatambui kama raia wa Kenya.

Share news tips with us here at Hivisasa

Wakaazi hao wa Garissa, ambao wamesajiliwa na shirika la UNHCR kama wakimbizi, walisema wanahitaji kutambuliwa na serikali kama wakenya kwa sababu wanaishi kwa hofu ya kukamatwa na kushtakiwa kwa sababu ya kukosa kadi za utambulisho.

Mama mmoja, Batula Siyat, aliyekuwa amebeba bango kubwa lenye maandishi, “UhuRuto tell us the way” alisema kuwa wanawe walinyimwa kadi hizo muhimu kwa sababu amesajiliwa na shirika la UNHCR kama mkimbizi. Alisema kuwa mwanawe wa kwanza hakukubaliwa kujiunga na chuo kikuu kwa sababu ya kukosa kitambulisho.

Maandamano hayo ambayo yaliongozwa na kiongozi wa wadi ya Galbet, Ibrahim Ali na kiongozi wa vijana, Abdirizak Ismail ilianzia kwenye barabara ya Kismayu na kuelekea hadi kwenye ofisi ya Kamishna wa Kaunti ya Garissa.

Akiwahutubia katika ofisi hizo, Ismail alisema kuwa wanapigania haki zao kama wakenya wengine na ya kuwa wana haki ya kusajiliwa bila ubaguzi. Alisema kuwa ni jukumu la rais kuwasaidia kutatua shida hilo.

“Licha ya kuwa wakenya wengine wanapata kitambulisho katika sehemu zingine kwa urahisi, mambo hapa ni tofauti,” alisema Ismail.

Akiwahutubia waandamanaji hao, kamishna wa kaunti alisema kuwa atafanya kikao na machifu ili kuhakikisha kuwa tatizo hilo la kitambulisho inasuluhishwa mara moja. Alielezea kuwa atafanya uchunguzi ili apate kujua ni kwa nini tatizo hilo lilitokea.