Wakaazi wanaopakana na msitu wa Mlima Menengai, eneo bunge la Bahati, katika kaunti ya Nakuru, waliandamana Jumatatu wakilalamikia kuhangaishwa na askari mmoja wa ulinzi wa msitu, kwa madai ya kutompa hongo.
Wakibeba mabango na matawi, wakaazi hao walielekea katika ofisi za shirika la KFS wakisema afisa huyo waliyemtambua kwa jina la utani kama ‘Shuguli’ amekuwa na mazoea ya kuchapa wakaazi wasio na hatia, huku akidaiwa kupapasa mwili akina mama wanaoenda msituni humo kutafuta kuni.
“Askari huyo wa KFS ametishia kuua watu kadhaa, na Jumapili usiku alikuwa anataka kupiga kijana mmoja risasi kwa sababu amekataa kutoa mia mbili lakini akaogopa watu waliojitokeza. Kuna mwingine mwaka jana (2015), aliua kijana anaitwa Kamau, na hakuna haki ilitendeka,” John Wanyoike alisema.
“Sisi tuna ghadhabu kwa sababu ‘Shuguli’ na wenzake walipiga msichana pale kwa msitu hadi akazirai baada ya kumshika shika kifua,” Monica Mwangi aliongeza .
Wakaazi hao walitoa malalamishi hayo kwa afisa mkuu wa msitu eneo hilo Erastus Mugo, wakisema ‘Shuguli’ huwa harudishi bunduki yake ofisini, jambo linalowafanya kuhofia inatumiwa kwa uhalifu.
“Shuguli must go. Kwa sababu tunahofia hiyo bunduki yake anayoweka kwa mtu nyumbani.”