Wakaazi wa Maili Kumi wanaopakana na kituo kimoja cha burudani kwa jina Joska Bar & Restaurant wameadika barua kwa utawala wa eneo hilo, wakitaka klabu hicho kufungwa kutokana na sababu kadhaa ikiwemo ukosefu wa usalama.
Barua ambayo mwandishi huyu amepata iliandikwa na kutiwa saini na wakaazi 27 mnamo tarehe 27 mwezi jana, na kutumwa kwa mkuu wa polisi wa Bahati, ambapo nakala yake imepewa pia OCPD wa Nakuru kaskazini Duncan Nguthu, naibu kaunti kamishna eneo hilo, kamanda wa askari wa utawala Nakuru kaskazini, na chifu wa kata ya Bahati, pamoja na mbunge Kimani Ngunjiri.
Barua hiyo inasema wakazi wa kijiji cha Guthera wamekuwa wakikabiliwa na matatizo yafuatayo kutokana na uwepo wa klabu hicho na hoteli: Kelele za saa 24 siku saba kwa wiki, kwa muda wa miezi minne iliyopita kutokana na disko kinyume na matakwa ya mamlaka ya kudhibiti mazingira nchini yaani NEMA.
Pili barua hiyo inataja kuwa watoto wao wengine ambao hawajafikisha miaka 18 wanauziwa sigara pamoja na pombe kwenye klabu hicho.
Aidha, wanasema usalama umezorota sana eneo hilo kutokana na uuzaji huo wa pombe, kiasi cha mama mmoja kubakwa mnamo tarehe 22 Machi mwaka huu, kisa kilichoripotiwa katika kituo cha polisi cha Bahati.
“Ubakaji huu ulitekelezwa na vijana walevi kutoka klabu cha Joska. Uuzaji wa bhangi unafanyika mchana hadharani na kuhatarisha usalama wetu,” barua hiyo inasema.
Mwenyekiti wa kijiji hicho Patrick mwaniki kwa upande wake alisema vijana wageni wamefurika kijiji hicho kutokana na klabu hicho, jambo linalohatarisha uhusiano bora pamoja na mpango wa nyumba kumi.
“Tungetaka bodi ya kudhibiti vileo nchini NACADA, na kamati inayotoa leseni za uuzaji wa vileo katika kaunti kufutilia mbali leseni ya klabu hicho,” akasema bwana Mwaniki.
Hata hivyo, naibu kaunti kamishna wa Nakuru kaskazini bwana Mutua alisema hajapokea rasmi barua hiyo, ila amepata kuskia kuihusu.
“Hatujaanzisha uchunguzi kwa sababu mwenyewe sijapokea barua hiyo, niliskia tu kutoka kwa wadokezi wangu, lakini Jumatano ijayo tunafanya mkutano wa usalama, na hapo tutazungumzia barua hiyo ikiwezekana tutafika katika kijiji hicho,” alisema afisa huyo.