Vijana wengi kaunti ya Mombasa bado hawajajitokeza na kuunda makundi ya kibiashara ili kufaidi fedha kutoka kwa hazina ya Uwezo Fund zilizotolewa na serikali ya kitaifa.
Inadaiwa vijana wameshindwa kuunda makundi ili kujisajili kama inavyohitajika kwani baadhi yao walidhani kuwa fedha hizo zitatolewa kwa watu binafsi.
Akiongea na mwandishi huyu katika afisi yake siku ya Jumatano, afisa wa mawasiliano katika eneo bunge la Mvita Eugine Omino alisema kiasi kikubwa cha fedha bado kimesalia katika kaunti za hazina hiyo.
“Tumetumia shilingi milioni 9 katika miradi tuliosajili kufikia sasa na bado tumesalia na shilingi milioni 5 katika akaunti ambazo hazijatumika lakini tunashangaa watu wametulia tu,” alisema Omilo.
Aidha afisa huyo anahimiza vijana na akina mama kujitokeza zaidi na kusajili makundi yao ili kupata fedha hizi na kujiendeleza.
Wakati uo huo, afisa huyo alisema kuwa eneo bunge la Mvita limesajili makundi 52 huku wengi wao ikiwa ni vijana ambao tayari wameanzisha biashara mbalimbali.
Omilo alisema kuwa mara kwa mara kamati maalum ikiongozwa na mbunge wa eneo hilo Abdulswamad Sharif Nassir hutembelea makundi hayo na kuangalia biashara wanazofanya.
Katika mradi huo uliozinduliwa rasmi na Rais Uhuru Kenyatta Septemba mwaka wa 2013, vijana, akina mama au walemavu wanatakiwa kujiunga katika makundi ya watu 10 au zaidi na kisha kusajili makundi hayo kabla kupewa fedha hizo.
Kila kundi linapewa mkopo wa kiasi cha shilingi elfu 50 na zaidi ili kuanzisha biashara wanazonuia kufanya.