Wakazi wanaotumia kivuko cha feri cha Likoni wamelalamika kukwama kwa mashini za kukagua mizigo katika kivuko hicho.
Wakiongea na Mwanahabari huyu mjini Mombasa, wakazi hao wamesema kuwa shida hiyo imechukua zaidi ya miezi miwili sasa tangu mashini hizo kuharibika na kusababisha msongamano wa abiria wanapovuka kwa ukaguzi kabla ya kuabiri feri.
Wakazi hao wamewataka wasimamizi wakuu wa shirika la huduma za feri nchini kuingilia kati swala hilo na kurekebisha mashini hizo sambamba na kupunguza msongamano katika sehemu hizo.
Aidha wamewataka wasimamizi wa shirika hilo la huduma za feri kutafuta mbinu mbadala za wakazi wanaotumia kivuko hicho kukaguliwa pamoja na mizigo yao iwapo mashini hizo hazitosaidia ili kupunguza msongamano.
"Tunawataka wasimamizi wakuu wa shirika la huduma za feri kuingilia kati swala hilo na kuboresha hali hiyo ili kupunguza msongamano katika kivuko hicho," alisema moja wa wakazi hao, James Fondo.
Maelezo ya picha:
Wakazi wakitumia eneo la ukaguzi katika kivuko cha feri cha Likoni mjini Mombasa. Wakaazi hao wamelalamikia huduma duni katika maeneo hayo.