Wakazi wa Mariakani wamelalamikia ukosefu wa ajira kwenye kampuni zinazoendesha biashara zao huko Mariakani licha ya eneo hilo kuwa miongoni mwa miji iliyona wawekezaji wakubwa nchini.

Share news tips with us here at Hivisasa

Wakazi hao wanasema kuwa licha ya kampuni kubwakubwa kuendesha biashara zao eneo hilo, nafasi za kazi ambazo hutangazwa kila mara na kampuni hizo huishia kuwafaidi wananchi wasio wakazi wa maeneo hayo.

Kulingana na Juma Chitole mkazi wa Mariakani, anasema amekuwa akienda kutafuta kazi ya udereva katika kampuni mbalimbali eneo hilo lakini hata wanapotoa vyeti vya kuonyesha tajriba ya kazi hiyo, kampuni hizo huishia kuwaajiri watu wa maeneo tofauti na mariakani huku wakazi wa maeneo hayo wakijazana kwenye malango makuu ya kampuni hizo wakisubiri majibu kutoka kwa wakurugenzi wakuu.

Chitole anasema kumekuwa na desturi ya baadhi ya kampuni kuwaajiri watu wanaowajua wala sio kulengana na vyeti vya nafasi za kazi walizosomea kwani kila wakati kunapotangazwa nafasi kama vile kumi za kazi ya udereva, huwa kunao watu mahususi walioratibiwa kuchukua nafasi hizo na kwamba hatua ya kutangaza huwa ni mojawapo njia za kuwafumba macho kuwa kuna utandawazi katika kuajiri wafanyakazi kwenye kampuni hizo.

Ann Kavuna mkazi wa Kokotoni Mariakani, anasema amekuwa akitafuta kazi ya ukatibu kwenye kampuni mbalimbali mjini mariakani ila jambo la kushangaza ni kwamba yeye hupita maswali yote ya usaili ila hajawai kuitwa kuanza kazi na hata anapoenda kufuatilia anaambiwa kazi hiyo ilishachukuliwa na mwenzake ambaye si mkazi wa maeneo hayo.

Kwa upande wake mwakilishi wa wadi ya Mariakani Said Mwachenda anasema kumekuwa na kipindi ambapo zaidi ya madereva kumi wa lori aina ya trela waliletwa kutoka Nairobi na kutwaa nafasi za kazi huku mkazi wa Mariakani akiendelea kutengwa, jambo ambalo amesema ni kinyume cha katiba.

Aidha amewataka vijana na wakazi wa mariakani kwa ujumla kuendelea kutafuta ajira kwenye kampuni hizo huku naye akiendelea kushauriana na mabwenyenye wa kampuni hizo jinsi ya wakazi hao watakavyapata ajira ili kujiendeleza maishani.