Wakaazi wa eneo bunge la Bahati wamemtaka mbunge wao Kimani Ngunjiri kuchimba visima vya maji ili kuwaepushia uhaba mkubwa wa maji unaowakumba.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wakiongozwa na Chifu wa lokesheni ya Kiamaina Arnold Maina, wakaazi hao walisema kuwa maji yanayosambazwa na shirika la kusambaza maji mjini Nakuru (NAWASSCO) hayawezi kutosha matumizi yao ya kila siku.

Walisema kuwa NAWASSCO huwasambazia maji kwa siku tatu kwa wiki hali waliyosema inawaacha na uhaba mkubwa wa mji huku wakitegemea wachuuzi wanaowauzia maji kwa bei ya juu.

“Tunamuomba mheshimiwa Ngunjiri atuchimbie visima hapa ili tuweze kupata maji kwa urahisi kwa sababu hili tatizo limekuwa hapa kwa muda mrefu. Wakati wa ukame tunasumbuka sana na tunatumia pesa nyingi kununua maji kutoka kwa wachuuzi. Tukiwa na visima vingi basi hili tatizo litatuondokea,” alisema chifu Maina.

Chifu huyo alipendekeza kuwa  itakuwa vyema iwapo visima hivyo vitachimbwa katika kila shule ya umma na vilevile katika makanisa ambapo wakaazi watavifikia kwa urahisi.

“Iwapo tunaweza kupata kisima kimoja katika kila shule na kanisa itakuwa vyema zaidi kwa sababu kwenye vituo hivyo, wakaazi watavifikia kwa urahisi,” aliongezea Maina.

Na akiwajibu wakaazi hao mwenyekiti wa bodi ya maendeleo katika eneo bunge la Bahati Mwangi Njue alisema kuwa tayari wana mipango ya kuchimba visima katika shule zote za umma katika eneo bunge hilo kuanzia kipindi cha matumizi ya fedha za serikali cha mwaka 2015/2016.

“Tuna hiyo mipango ya kutatua tatizo la uhaba wa maji hapa Bahati. Tayari mwanakandarasi atakaye fanya kazi hiyo ametambuliwa na bodi,” alifichua Njue.

Wakaazi hao walikuwa wakiongea katika shule ya msingi ya Kiamaina, siku ya Jumapili wakati wa shuguli ya matibabu ya bure ya macho yalioandaliwa na shirika la Lions la Nakuru.