Wananchi katika kaunti ya Nyamira wameonywa vikali dhidi ya kuandikisha watoto mayatima na ambao wana familia ambayo inajiweza na ambayo inaweza kulea watoto hao bila shida yoyote.
Akiongea wakati wa sherehe za kuadhimisha siku kuu ya mayatima nchini, afisa mkuu wa kitengo hicho katika kaunti hiyo Alice Oyioka alisema kuwa wamekuwa wakikumbana na visa vingi vya aina hiyo, jambo ambalo linawanyima mayatima maskini nafasi ya kusaidiwa.
Aidha, Oyioka ameongeza kuwa wale wasichana au wanawake ambao huzaa kabla ya kuolewa wawatambue baba za watoto wao ili wachangie katika kulea watoto hao badala ya kuandikishwa kama mayatima ilihali wazazi wao wote wako hai.
"Tumegundua watoto wengi ambao tunaandikisha kama mayatima wana wazazi wao, tofauti tu ni kwamba mama zao hawataki kuwatambua baba zao ili nao waonekane ikiwa wana uwezo wa kuchangia katika malezi," aliongeza Oyioka.
Afisa wa watoto katika kaunti ndogo ya Nyamira Purity Lamont amewahimiza wananchi kuwaleta watoto ambao kwa bahati mbaya wamekuwa mayatima ili waweze kusaidiwa badala ya kuwapeleka kuachiliwa kuwa mayaya, kuwaoza ama kuwaacha nyumbani na kukosa mahitaji ya muhimu kama elimu.