Seneta mteule wa chama cha Alliance Party of Kenya, Beatrice Elachi, amewataka wakazi wa maeneo ya magharibi ya Kenya na Nyanza kuacha kujihusisha na siasa kuhusiana na swala la sukari nchini.
Mkataba wa sukari unaodaiwa uliafikiwa na Rais Uhuru Kenyatta na serikali ya Uganda, umeleta joto kali baina ya serikali ya Jubilee na chama cha upinzani cha Cord.
Akiongea katika hafla ya kikatholiki ya kuwaalika nyumbani wasimenari katika eneo la Ekerema katika eneo bunge la Bobasi, siku ya Alhamisi, Bi Elachi aliwaambia wanasiasa kuwa ni kinyume na maadili kuingiza siasa katika kila jambo linalofanywa na serikali kuu.
Aliwataka wananchi hasa kutoka eneo la magharibi ambalo ndilo limeathirika kufuatia swala hilo kuwa na subira na kuacha kuahadaiwa na wanasiasa ambao wanaweka maslahi yao mbele bila kuzingatia mkazi wa maeneo husika.
Alisema kuwa swala hilo la mkataba baina ya serikali ya Kenya na Uganda kuuza sukari katika nchi ya Kenya bado haujapitishwa.
Aliwaomba wanasiasa pamoja na viongozi kutoka eneo la Magharibi na lile la Nyanza kutafuta njia mwafaka na inayokubalika kisheria ya kujadili na kuangazia swala hilo.
Seneta huyo alisema kuwa swala hili lisipo shughulikiwa vizuri huenda likaleta uadui miongoni mwa wakenya wa kawaida.
“Wanasiasa sharti wajiepusha na masuala ya kuchochea watu ilhali shida ikitokea mwananchi wa kawaida ndiye uumia na wenye pesa na mamlaka uendelea kufurahia maisha huku nyinyi mkiteseka. Kwa hivyo, mujiepushe na siasa za kuwatenganisha,” alisema Elachi.