Wakazi wa eneo la Shika Adabu wametakiwa kutumia vizuri neti walizopewa na serikali kupitia kwa Wizara ya Afya mwaka jana, ili kujikinga na maambukizi ya malaria hasa nyakati za usiku wanapolala.
Haya yamejiri baada ya kubainika kuwa watoto na akina mama wengi wamekua wakitembelea kituo cha afya cha eneo hilo ila kupata matibabu ya ugonjwa wa malaria.
Akizungumza siku ya Alhamisi, muuguzi katika kliniki ya Shika Adabu Bi Sofia alisema kuwa baadhi ya wakazi wa eneo hilo walitumia neti hizo kwa shughuli zingine.
"Watu walijisajili wakapewa neti za kujikinga dhidi ya mbu lakini wengine walizitumia kwa kazi zingine kama ufugaji kuku. Jamani neti zilikuwa za kutumika nyakati za usiku na hasa wakati huu ambao majira ya mvua yanakaribia, kwani mbu huzaana kwa wingi,” alisema Bi Sofia, alipokua akitoa ushauri kwa akina mama hospitalini humo.
"Akina mama ndio wanafaa kuihimiza familia yao kulala ndani ya neti ili kuzuia mbu. Nawasihi tafadhali tahadhari kabla ya hatari,” alisema Sophia.
Muuguzi huyo aliongeza kusema kuwa watu wengi kwa sasa wamefika kituoni humo na dalili za ugonjwa huo na kuwataka wakazi kutumia neti hizo ipasavyo.