Wake wa magavana kutoka kaunti ya Kisii, Nyamira, Homabay, Siaya, Kisumu, Bungoma, Kakamega na Migori wamejitokeza kuwataka wakenya kukumbatia amani na utangamano kabla ya uchaguzi mkuu ujao.

Share news tips with us here at Hivisasa

Wakihutubu katika hafla yakuchangisha pesa za ujenzi wa makao rasmi ya watawa wa paroko ya kanisa katholiki la Nyamira wake hao walisema kuwa yafaa wakenya kukumbatia amani ili kuepukana na uwezekano wakuwepo mafarakano ya kisiasa.

"Kwa niaba ya wake wa magavana wote tulio hapa hii leo ningependa kuwapa changamoto wakenya kuishi pamoja kwa amani tunapoelekea kwenye uchaguzi mkuu ujao kwani taifa hili ni kubwa kutushinda sisi," alisema Mke wa gavana wa Kisii Bi Elizabeth Ongwae.

Bi Ongwae aidha alisihi vyama vya kisiasa nchini kuandaa mazungumzo ili kusuluhisha mzozo unaokumba Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini (IEBC).

"Nadhani ni jambo la muhimu iwapo vyama vya kisiasa vitafanya mazungumzo ya pamoja na tume ya IEBC ili kusuluhisha mzozo unaokumba tume hiyo kuhusiana na Shinikizo za kutaka tume hiyo kuondoka ofisini kwa maana Kenya ni kubwa kuliko mwanasiasa yeyote," aliongezea Bi Ongwae.