Mwenyekiti wa baraza la Maimamu na maubiri ya Kiislamu katika Kaunti ya Uasin Gishu amewasihi wananchi kutoka madhehebu mbali mbali kuja pamoja na kuomba ili Mungu awape mvua.
Akizungumza na wanahabari katika hoteli moja siku ya Jumatano mjini Eldoret, Abubakhar Bini aliwasihi viongozi na wananchi kwa jumla waungane mikono kwa kuomba sana kwani ukame umezidi na huu unaweza kuwa ni pigo toka kwa Mwenyezi Mungu.
Alizidi kusema kuwa kama kuna kiongozi aliye na makosa, haswa wanasiasa waombe msamaha na waungane na wenzao kwa minajili ya kuombaea mvua katika nchi yetu.
“Haya sio maneno yangu, bali ni kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Naomba Wakenya kwa jumla kutubu dhambi zao na kumrudia Mungu ili tupate baraka ya mvua,” alisisitiza Bini.
Hii ni kufuatia ongezeko la ukame katika Kaunti mbali mbali haswa Kaskazini mwa nchi ya Kenya.
Aidha, aliongeza kwamba kila mmoja anafaa kuwajibika na kuomba kwani hali ikiendelea kudorora basi watu wote wataangamia.
“Wale wasiokua na dini na wale wanaoshiriki kwa dini inafaa waungane mikono sababu adhabu itapata aliyekua na asiyekua,” aliongeza Bini.
Vile vile amesihi serikali ijiandae vilivyo kwa msimu huu wa kiangazi kutafuta chakula ili wakati utakapofika wawe tayari kuokoa maisha ya wakenya wengi ambao wanaweza kujipata kwenye janga hilo.
Dalili tayari inaonyesha kwamba mvua bado uko mbali na hivyo basi inafaa serikali iweke mikakati madhubuti ili iweze kukabiliana na janga la njaa na ukosefu wa maji wakati utakapofika.