Huku baadhi ya wakenya wakisherehekea siku kuu ya Madaraka wengine hawakuona umuhimu wa sherehe hizo.
Ambao waliona umuhimu wa siku hii walitembea katika mahali pa burudani na familia zao pamoja na marafiki huku ambao hawakuona haja ya siku hii wakiendelea na kazi zao za kutafuta lishe.
Nicholaus Abuto muuzaji nguo katika soko la Kibuye kaunti ya Kisumu ambaye alikuwa anaendelea na kazi yake alisema kuwa haoni haja ya siku hiyo.
Hii ni siku ya walionazo lakini wengine kama mimi ni lazima ni fungue biashara yangu angalau niweze kujipatia lishe,” alisema Abuto.
“Kenya hii wachache ndio wanaoona uzuri wa madaraka kwa sababu wametengeneza mali na wanaweza kuona umuhimu wa siku hii,” aliongeza Abuto.
Wachuuzi waliokuwa wakiuza bidhaa zao kando mwa barabara za jiji walisema kuwa serikali inastahili kuinua maisha ya kila mwananchi ili kila mmoja aweze kufurahia matunda ya uhuru na kuadhimisha siku kuu.
“Kupitia serikali za Kaunti serikali kuu sasa inao wakati mzuri sana wa kuinua maisha ya wananchi wake kwa kusambaza rasilimali mashinani ili kila mmoja aweze kufurahia matunda ya uhuru,” alisema Titus Obara.