Afisi ya mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma imetakiwa kufafanua iwapo mauaji yaliyotokea katika Kituo cha polisi cha Central ni ya kigaidi ama ya kiholela.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Mbugua Mureithi, wakili wa Haniya Saggar, ambaye ni mke wa marehemu Sheikh Aboud Rogo, ameitaka afisi ya mkuu wa mashtaka ya umma kuwaelezea Wakenya wazi wazi kuhusu chanzo cha mauaji ya wasichana watatu waliopigwa risasi katika kituo hicho cha polisi na kisha kudaiwa kuwa magaidi.

“Ni jambo la kushangaza kusikia kuwa wasichana wadogo eti wamevamia kituo cha polisi kwa visu. Kwanini polisi wasingewashika na kuwashtaki? Mbona waliwapiga risasi na kuwaua ikizingatiwa polisi wanaujuzi wa kukabiliana na wahalifu hata bila kutumia bunduki,” alisema Mbugua.

Wakili huyo amiembia Mahakama ya Shanzu kuwa polisi kote ulimwenguni wanatekeleza mauaji ya kiholela kisha kudai kuwa waathiriwa walikuwa magaidi.

“Tunataka ufafanuzi wa kina kuhusu mauaji haya. Polisi kote duniani wanatekeleza mauaji ya kiholela kisha kuyataja kama ya ugaidi,” alisema Mbugua.

Mbugua alidai kuwa mauaji hayo yalikuwa ya kiholela dhidi ya Wakenya wasiokuwa na hatia, na wala sio ya kigaidi kama inavyodaiwa na polisi.

“Vijana wengi wanapoteza maisha kwa kupigwa risasi, huku wakisingiziwa kuwa ni magaidi. Jambo hili limewafanya vijana kuishi kwa hofu kubwa ya kuangamizwa,” alisema Mbugua.

Wakati huo huo, ameongeza kuwa hadi sasa upande wa utetezi hauna ufahamu kuhusu mashahidi wa kesi hiyo.

Haniya Saggar, Nastaheno Ali Thalili, Luul Ali Thahil na Zamzam Abdi Abdallah wanadaiwa kukosa kutoa habari kwa polisi kuhusu uvamizi wa Kituo cha polisi cha Central.