Baada ya tume ya uchaguzi na mipaka nchini kujikokota kuthibitisha saini za wafuasi wa muungano wa CORD waliokuwa wamepeana saini zao ili kuruhusu mlengo huo kufanya kura ya maamuzi, sasa wakili Victor Swanya amejitokeza kusema kwamba tume ya IEBC ina nia ya kusambaratisha juhudi za muungano wa CORD.
Akiwahutubia wanahabari mjini Nyamira siku ya Jumatano, Swanya alisema kuwa kuchelewa kwa tume ya IEBC kuthibitisha saini hizo zaidi ya millioni moja ni mbinu IEBC inatumia ili kuhujumu juhudi za mlengo wa CORD kutaka kura ya maamuzi kufanyika.
"Hali hii ya tume ya IEBC kuendelea kujikokota kuhusiana na uthibitishaji wa saini za wakenya wanaotaka kura ya maamuzi kufanywa ilu kurekebisha baadhi ya vipengee vya rasimu ya katiba ni mbinu tume ya IEBC inatumia ili kuhujumu juhudu za CORD kutaka kura ya maamuzi kufanyika kabla ya uchaguzi mkuu ujao," alisema Swanya.
Swanya aidha aliongeza kwa kuwarahi wakenya kuwachagua viongozi kwa misingi ya rekodi za utendakazi wao na wala sio kwa kuegemea vyama vya kisiasa.
"Kumekuwa na hii tamaduni ya viongozi kuchaguliwa kutokana na milengo ya kisiasa wanayoegemea, ila ni ombi langu kwa wakenya kuhakikisha kwamba wanawachagua viongozi wa nyadhifa za kisiasa kwa kuzingatia rekodi za utendakazi wao," aliongezea Swanya.