Wakili Kemosi Mogaka ameisihi serikali kuweka mikakati ya kuhakikisha shule zote za umma zimeunganishwa na nguvu za umeme kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka ujao.
Kwenye mahojiano ya kipekee kwa njia ya simu siku ya Jumatatu, Mogaka alisema kuwa yafaa serikali iziunganishie shule zote za msingi umeme ili kuziwezesha kutoa huduma kwa urahisi.
“Ni jukumu la serikali kuhakikisha kuwa shule zote za umma zinatoa huduma bora za masomo, na hilo haliwezekani iwapo shule hizo hazitounganishiwa stima kwa wakati unaofaa," alisema Mogaka.
Mogaka aidha aliongeza kwa kuwataka walimu wa shule za umma kuhakikisha kuwa wanaotoa huduma za masomo zinazostahili il kuinua viwango vya elimu katika shule za umma.
“Kuna shule za msingi zaidi ya elfu moja nchini na tayari serikali ya kitaifa imeunganisha shule 450 na nguvu za umeme, na isiwe kwamba shule hizo zinapata umeme bila ya walimu kujitolea kuhakikisha wanafunzi wanapata manufaa ya nguvu za umeme," aliongezea Mogaka.