Kufuatia hali ya Rais Uhuru Kenyatta kukosa kuzungumzia suala la mzozo wa umiliki wa kisiwa cha migingo kati ya serikali ya Uganda na Kenya, mwanasiasa Victor Swanya amejitokeza kukashifu vikali hali hiyo.
Kwenye mahojiano mapema Jumanne, Swanya alisema kwamba ni jambo la aibu kwamba Rais Kenyatta amelinyamazia suala hilo huku ikibainika wazi kwamba kisiwa cha Migingo kiko katika himaya ya taifa hili.
"Ni jambo la aibu kwamba Rais Kenyatta anaweza fanya kikao na rais wa Uganda Yoweri Museveni na akose kuzungumzia suala la umiliki wa kisiwa cha migingo, ikizingatiwa kwamba kisiwa hicho kipo hapa nchini," alishangazwa Swanya.
Swanya aidha aliongeza kwa kuziomba serikali ya Kenya na ile ya Uganda kuwatafuta masoroveya wenye tajriba ya hali ya juu kupima eneo hilo la kisiwa cha Migingo ili kusuluhisha mzozo huo wa muda kwa haraka.
"Ombi langu ni kwa serikali ya nchi hii na ile ya Uganda kuwatafuta masoroveya wenye tajriba ili kupima kisiwa cha migingo na kubaini hasa iwapo kipo humu nchini au Uganda," aliongezea Swanya.