Wakili mmoja katika Mahakama kuu ya Mombasa amepinga hatua ya taifa la Kenya kutaka kuwaondoa wakimbizi katika kambi za Dadaab na Kakuma.

Share news tips with us here at Hivisasa

Pascal Nabwana, alisema kuwa hatua hiyo ni ukiukaji wa haki za binadamu ikizingatiwa wakimbizi hao hawana sehemu mwafaka ya kuishi.

Akizungumza na mwandishi huyu siku ya Jumanne, katika jengo la Mahakama ya Mombasa, Nabwana alisema kuwa usalama wa wakimbizi hao utadorora sana, ikizingatiwa kuwa itakuwa vigumu kwao kupata maakazi mbadala kwa haraka.

“Kenya inastahili kushirikiana na kitengo cha umoja wa mataifa kinachoshughulikia wakimbizi ili kutafuta suluhu mwafaka badala ya kufunga kambi za wakimbizi za Kakuma na Daadab,” alisema Nabwana.

Kauli hii inajiri baada ya Shirika la Umoja wa Mataifa linalosimamia wakimbizi UNHCR, kuitaka serikali ya Kenya kubatilisha msimamo wake wa kutaka kuzifunga kambi hizo mbili za wakimbizi.