Wakili kutoka Kaunti ya Mombasa amepinga pendekezo la kufunguliwa kwa bahasha ya Waki ambayo inadaiwa kuwa na majina zaidi ya washukiwa wa ghasia za baada ya uchaguzi wa mwaka 2007.
Akizumgumza na mwandishi huyu siku ya Jumanne katika Mahakama ya Mombasa, Pascal Nabwana, ambaye pia ni mchanganuzi wa maswala ya kisiasa, alisema kuwa kufunguliwa kwa bahasha ya Waki kutaongeza joto la kisiasa nchini, jambo alilosema kuwa litalemaza shughuli za maendeleo.
“Kufunguliwa kwa bahasha hiyo pia kunaweza kuleta ukabila miongoni mwa jamii hasa iwapo jamii moja ama mbili zitatajwa katika bahasha hiyo,” alisema Nabwana.
Kauli hii inajiri baada ya baadhi ya wananchi na viongozi pamoja na mashirika ya kutetea haki za kibinadamu kutaka kuwekwa wazi kwa majina yaliyomo kwenye ripoti hiyo ya Waki.
Haya yanajiri baada ya mahakama ya jinai ya ICC kuwaondolea mashtaka Naibu Raisi William Ruto pamoja na mwanahabari Joshua Arap Sang.