Itakuwa vigumu sana kwa Kenya kukwepa mtego wa kuandamwa na mahakama ya kimataifa ICC hata ikifaulu kujiondoa katika mkataba wa Roma uliobuni mahakama hiyo.
Haya ni maneno ya wakili Victor Kapiyo. Kapiyo alisema inatokana na mikataba ya kimataifa kuhusu haki za kibinadamu ambayo Kenya ni mwanachama na ambayo hairuhusu ukiukaji wa haki za kibinadamu.
‘‘Sheria za dunia zinasema kwamba hata nchi ikijitoa katika makataba kama huo bado hiyo sheria inaweza kutumika na sasa haijalishi kama Kenya itajitoa au la,” alisema Kapiyo.
Aidha, mtetezi huyo wa haki za kibinadamu alieleza ili taifa lolote lile ijiondoe katika mkataba wa Roma, itachukua muda mrefu ikiwemo mswada ambayo ni sharti uwasilishwe katika bunge la kitaifa kwa mjadala kabla ya kuidhinishwa.
“Ni lazima kuwasilishwe mswada wa kijiondoa katika huo mkataba na upitishwa na bunge la kitaifa. Mswada huo utatakikana kutiwa sahihi na rais na kuwasilishwa kwa umoja wa mataifa na pia kujadiliwa na utakapotiwa sahihi, basi tutakuwa tumejiondoa katika mkataba wa Roma,” aliongezea Kapiyo.