Baada ya tume ya mitihani ya kitaifa nchini KNEC kufutilia mbali matokeo ya mtihani wa kidato cha nne ya wanafunzi elfu tano, sasa wakili Denis Anyoka amejitokeza kushtumu vikali hatua hiyo. 

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Kwenye mahojiano kwa njia ya simu siku ya Jumanne, Anyoka alishangazwa na sababu iliyosababisha tume hiyo kufutilia mbali matokeo ya mtihani wa wanafunzi hao ilhali udanganyifu kwenye mitihani ulishuhudiwa kote nchini. 

"Ni jambo la kushangaza kwamba KNEC inaweza futilia mbali matokeo ya mtihani ya wanafunzi elfu tano pekee ilhali uhalali wa mtihani huo ulikumbwa na dosari kote nchini," alishangazwa Anyoka. 

Anyoka aidha alimpongeza waziri wa elimu nchini Fred Matiang'i kwa hatua ya kusimamisha kazi bodi nzima ya KNEC, huku akimtaka waziri huyo kuhakikisha kartasi za mitihani ya wanafunzi hao zinasahihishwa upya. 

"Ingelikuwa vizuri iwapo waziri Matiang'i angehakikisha kwamba kartasi za mtihani za wanafunzi walioathirika zinasahihishwa upya ili wanafunzi hao wapokee matokeo yao, ila pia ni pongezi kwake Matiang'i kwa kuwasimamisha kazi maafisa wakuu wa tume hiyo," aliongezea Anyoka.